Jumamosi asubuhi;
22.08.2026;
Luka 18:9-14
[9]Akawaambia mfano huu watu waliojikinai ya kuwa wao ni wenye haki, wakiwadharau wengine wote.
[10]Watu wawili walipanda kwenda hekaluni kusali, mmoja Farisayo, wa pili mtoza ushuru.
[11]Yule Farisayo akasimama akiomba hivi moyoni mwake; Ee Mungu, nakushukuru kwa kuwa mimi si kama watu wengine, wanyang’anyi, wadhalimu, wazinzi, wala kama huyu mtoza ushuru.
[12]Mimi nafunga mara mbili kwa juma; hutoa zaka katika mapato yangu yote.
[13]Lakini yule mtoza ushuru alisimama mbali, wala hakuthubutu hata kuinua macho yake mbinguni, bali alijipiga-piga kifua akisema, Ee Mungu, uniwie radhi mimi mwenye dhambi.
[14]Nawaambia, huyu alishuka kwenda nyumbani kwake amehesabiwa haki kuliko yule; kwa maana kila ajikwezaye atadhiliwa, naye ajidhiliye atakwezwa.
Mungu huwainua wanyenyekevu;
Yesu anatoa mfano wa Farisayo na mtozaushuru waliopanda hekaluni kusali. Mafarisayo lilikuwa ni kundi la wayahudi washika dini, walioifuata torati ya Musa. (Mat 3:7, Marko 2:16, Luka 5:17, Yoh 1:24).
Lakini walimtesa sana Yesu na kumuumiza. Lakini kwa upande mwingine, waliukubali ufufuko wa wafu, kitu ambacho Masadukayo hawakukikubali!
Farisayo alijiona mwenye haki, akaomba kwa kujisifia, lakini mtozaushuru aliomba toba kwa Mungu.
Katika mfano huu tunaweza kuona kuwa;
1.Njia mbaya ya kumkaribia Mungu ni kwa kuzitegemea kazi zako mwenyewe.
Yaani usije ukafikiri utamkaribia Mungu kwa sababu ya unayoyafanya! Hata Farisayo alikuwa anafanya mengi mazuri kuliko wewe!
Tunapomkaribia Mungu, sharti tutambue kuwa tu wenye dhambi, na tumkaribie kwa unyenyekevu!
Kwanza huna haja ya kutaja kazi zako mbele za Mungu kwa sababu ni wajibu wako! Yaani ni wajibu wako kutenda mema (+Bagonza)
Usiwe kama Farisayo, usijitape, acha sifa, Mungu haitaji maelezo ya sifa zako, fanya kazi yake kwa bidii na uaminifu, na uende mbele zake kwa unyenyekevu.
-Watu wanaokwenda kwa Mungu wakitegemea kazi zao wenyewe, wanajiamini wao wenyewe.
-Watu wanaojaribu kumwendea Mungu kwa kazi zao wenyewe wanajiona wao bora kuliko wengine.
-Watu wanaomwendea Mungu kwa kuzitegemea kazi zao wenyewe, wanajilinganisha wenyewe na wengine, na sio kujipeleka kwa Mungu.
-Watu wanaokwenda kwa Mungu kwa kuzitegemea kazi zao wenyewe, wanaangalia mambo ya kiMungu kwa nje, na sio mioyo yao mbele ya Mungu.
Acha njia mbaya, mwendee Mungu kwa unyenyekevu.
2.Njia sahihi ya kumwendea Mungu, ni kutambua kuwa tu wenye dhambi, na kuishi kwa toba.
Watozaushuru;
Walionekana wasaliti kwa kutumikia Warumi
Walionekana waovu, maana kuna wakati walitoza kinyume.
Walionekana watenda dhambi kutokana na aina ya kazi yao.
Sasa huyu tuliyemsoma, aweza kuwa na dhana mbili;
Yaani inawezekana alitambua kuwa yeye kama mwanadamu, ni mwenye dhambi, hivyo anahitaji toba wakati wote, au, inawezekana alitoza kodi kinyume na sheria, au vyote viwili
Funzo analotupa huyu ndugu ni kuwa, sisi ni wenye dhambi tu, ni wajibu wetu kufanya toba wakati wote.
-Watu wanaotubu dhambi zao wanatambua kuwa lazima watubu.
-Watu wanaotubu dhambi zao kwa unyenyekevu wanajua kabisa kuwa Mungu wetu anastahili kunyenyekewa. Wewe ni mmojawapo?
3.Mwenye dhambi anapomwendea Mungu kwa unyenyekevu, kwa neema Mungu anampokea.
Yesu anasema kuwa mtoza ushuru alienda nyumbani kwake akiwa amesamehewa. Pamoja na kwamba alifanya toba, hakuacha kuwa mnyenyekevu.
Hapa tunakumbushwa kuuishi mfano wa mtoza ushuru aliyeenda mbele za Mungu akiomba toba kwa unyenyekevu.
Unyenyekevu ni tabia ya Mungu.
Wewe unayo?
Jumamosi njema
Heri Buberwa
