VIDEOS

Angalia picha mjongeo (Video) za ibada na matukio maalum ya Usharika hapa https://m.youtube.com/@AZANIAFRONTCATHEDRAL

Date
Reading
Waebrania 11:32-40

Alhamisi asubuhi tarehe 15.10.2026

Waebrania 11:32-40

[32]Nami niseme nini tena? Maana wakati usingenitosha kuleta habari za Gideoni na Baraka na Samsoni na Yeftha na Daudi na Samweli na za manabii;

[33]ambao kwa imani walishinda milki za wafalme, walitenda haki, walipata ahadi, walifunga vinywa vya simba,

[34]walizima nguvu za moto, waliokoka na makali ya upanga. Walitiwa nguvu baada ya kuwa dhaifu, walikuwa hodari katika vita, walikimbiza majeshi ya wageni.

[35]Wanawake walipokea wafu wao waliofufuliwa. Lakini wengine waliumizwa vibaya hata kuuawa, wasikubali ukombozi, ili wapate ufufuo ulio bora;

[36]wengine walijaribiwa kwa dhihaka na mapigo, naam, kwa mafungo, na kwa kutiwa gerezani;

[37]walipigwa kwa mawe, walikatwa kwa misumeno, walijaribiwa, waliuawa kwa upanga; walizunguka-zunguka wakivaa ngozi za kondoo na ngozi za mbuzi; walikuwa wahitaji, wakiteswa, wakitendwa mabaya;

[38](watu ambao ulimwengu haukustahili kuwa nao), walikuwa wakizunguka-zunguka katika nyika na katika milima na katika mapango na katika mashimo ya nchi.

[39]Na watu hao wote wakiisha kushuhudiwa kwa sababu ya imani yao, hawakuipokea ahadi;

[40]kwa kuwa Mungu alikuwa ametangulia kutuwekea sisi kitu kilicho bora, ili wao wasikamilishwe pasipo sisi.

Mwenye haki ataishi kwa imani;
Waraka kwa Waebrania sura ya 11 huongelea imani, ukionesha watu mbalimbali walivyoshinda kwa imani. Kitabu hiki huanza kwa kueleza maana ya imani (1-3). Huonesha mfano wa Habili, Enoko na Nuhu (4-7), Imani ya Ibrahim (8-22), Imani ya Musa (23-28) na sehemu ya mwisho huwaongelea mashujaa wengine wa Israeli walivyoshinda kwa imani (29-40) kabla ya kumsoma Yesu mwenyewe kuhusu imani (sura ya 12)
Leo asubuhi tunawasoma mashujaa wengine wa Israeli, waliokataa uovu kwa sababu ya imani, wakashinda. Hata walipojaribiwa na kupigwa, hawakumwacha Mungu. Walizima nguvu za moto, waliokoka na makali ya upanga, walikimbiza majeshi ya wageni,   walifunga vinywa vya simba n.k Waliovumilia walishinda.
Shida tunazopitia zisitutoe kwa Mungu, bali Imani yetu idumu katika Kristo, ndipo tutakuwa na mwisho mwema, yaani kushinda katika yeye. Usifikiri Mungu amekuacha, bali mtegemee yeye kwa imani utashinda. Siku njema.

Heri Buberwa