Jumanne asubuhi tarehe 25.08.2026;
Waamuzi 11:29-33
29 Ndipo roho ya Bwana ikamjilia juu yake Yeftha, naye akapita katika Gileadi na Manase, akapita na katika Mispa ya Gileadi, na kutoka hapo Mispa ya Gileadi akapita kuwaendea wana wa Amoni.
30 Naye Yeftha akamwekea Bwana nadhiri, akasema, Kwamba wewe utawatia wana wa Amoni mkononi mwangu kweli,
31 ndipo itakuwa ya kwamba, kile kitakachotoka katika milango ya nyumba yangu kunilaki, hapo nitakaporudi na amani kutoka kwa hao wana wa Amoni, kitu hicho kitakuwa ni cha Bwana, nami nitakisongeza kiwe sadaka ya kuteketezwa.
32 Basi Yeftha akavuka kuwaendea wana wa Amoni ili kupigana nao; naye Bwana akawaua mkononi mwake.
33 Akawapiga kutoka Aroeri hata kufikilia Minithi, miji ishirini, na mpaka Abel-keramimu, akawapiga kwa machinjo makuu mno. Basi hivyo wana wa Amoni walishindwa mbele ya wana wa Israeli.
Tutumie ndimi zetu kwa Utukufu wa Mungu;
Kiongozi wa Israeli, Yeftha, anaingia vitani na wana wa Amoni kwa nguvu ya Mungu. Yeftha anashinda vita hiyo, na kabla ya vita hiyo alitoa ahadi kwa Bwana kwamba akishinda vita, kila kitu ambacho kingetoka kwake kingekuwa sadaka ya kuteketezwa kwa Bwana. Mungu anawashindia Israeli kwa kuipiga miji ishirini na kuwatiisha waAmoni.
Somo linaonesha pamoja na Yeftha kuwa na kasoro (mst 1-10) bado Mungu alimtumia kuwashindia Israeli. Hii inatukumbusha kwamba pamoja na udhaifu wetu Mungu anatupokea na kutupa wokovu. Katika uovu wetu Mungu anatusamehe dhambi zetu. Ni kwa muktadha huo tunakumbushwa kumwamini na kumfuata daima, tukitenda yote kwa Utukufu wake. Amina
Siku njema
Heri Buberwa
