
Jumamosi asubuhi tarehe 14.11.2026;
Ufunuo wa Yohana 13:1-10
1 Kisha nikaona mnyama akitoka katika bahari, mwenye pembe kumi, na vichwa saba, na juu ya pembe zake ana vilemba kumi, na juu ya vichwa vyake majina ya makufuru.
2 Na yule mnyama niliyemwona alikuwa mfano wa chui, na miguu yake ilikuwa kama miguu ya dubu, na kinywa chake kama kinywa cha simba, yule joka akampa nguvu zake na kiti chake cha enzi na uwezo mwingi.
3 Nikaona kimoja cha vichwa vyake kana kwamba kimetiwa jeraha la mauti, na pigo lake la mauti likapona. Dunia yote ikamstaajabia mnyama yule.
4 Wakamsujudu yule joka kwa sababu alimpa huyo mnyama uwezo wake; nao wakamsujudu yule mnyama, wakisema, Ni nani afananaye na mnyama huyu? Tena ni nani awezaye kufanya vita naye?
5 Naye akapewa kinywa cha kunena maneno makuu, ya makufuru. Akapewa uwezo wa kufanya kazi yake miezi arobaini na miwili.
6 Akafunua kinywa chake amtukane Mungu, na kulitukana jina lake, na maskani yake, nao wakaao mbinguni.
7 Tena akapewa kufanya vita na watakatifu na kuwashinda, akapewa uwezo juu ya kila kabila na jamaa na lugha na taifa.
8 Na watu wote wakaao juu ya nchi watamsujudu, kila ambaye jina lake halikuandikwa katika kitabu cha uzima cha Mwana-Kondoo, aliyechinjwa tangu kuwekwa misingi ya dunia.
9 Mtu akiwa na sikio na asikie.
10 Mtu akichukua mateka, atachukuliwa mateka. Mtu akiua kwa upanga, atauawa kwa upanga. Hapa ndipo penye subira na imani ya watakatifu.
Mwenye kuvumilia hata mwisho ataokoka;
Mnyama kutoka baharini anaonekana na Yohana, ana vichwa na pembe kumi, vilemba kumi na majina ya makufuru. Inahusiana na wanyama wanne katika kitabu cha Danieli sura ya 7. Shetani anampa mnyama nguvu za kiti chake, mamlaka na uwezo mwingi. Mnyama mmoja anaumia kichwa, halafu anapona! Mnyama anaongea kufuru kuhusu Mungu kwa miezi 42, anafanya vita na watu wa Mungu. Kila ambaye jina lake halikuonekana kitabuni alimuabudu mnyama.
Wakristo wengi humtafsiri mnyama kama kitu kinachowakilisha adui katika maisha yote, wengine tangu historia (wakihusisha na himaya ya Rumi) wengine wakiona kama mwisho ujao wa mpinga Kristo. Mstari wa kumi unahitimisha somo kwa wito wa imani na uvumilivu kwa waaminio wapatao changamoto katika njia ya ufuasi. Tunaitwa kuwa wavumilivu katika imani ili tuwe na mwisho mwema. Amina
Siku njema
Heri Buberwa
Mlutheri
