Marko 7:31-37 - 24-08-2026

Date
Reading
Marko 7:31-37

Jumatano asubuhi 26.08.2026;

Marko 7:31-37

[31]Akatoka tena katika mipaka ya Tiro, akapita katikati ya Sidoni, akaenda mpaka bahari ya Galilaya, kati ya mipaka ya Dekapoli.

[32]Wakamletea kiziwi, naye ni mwenye utasi, wakamsihi amwekee mikono.

[33]Akamtenga na mkutano faraghani, akatia vidole vyake masikioni mwake, akatema mate, akamgusa ulimi,

[34]akatazama juu mbinguni, akaugua, akamwambia, Efatha, maana yake, Funguka.

[35]Mara masikio yake yakafunguka, kifungo cha ulimi wake kikalegea, akasema vizuri.

[36]Akawaonya wasimwambie mtu; lakini kadiri ya alivyozidi kuwaagiza, ndivyo walivyozidi kutangaza habari;

[37]wakashangaa mno kupita kiasi, wakinena, Ametenda mambo yote vema; viziwi awafanya wasikie, na bubu waseme.

Tutumie ndimi zetu kwa Utukufu wa Mungu;

Somo linaonesha kuwa Yesu alipofika Dekapoli walimletea kiziwi amponye. Walimsihi amwekee mkono. Bila shaka hapa kulikuwa na mazungumzo, kati ya Yesu na waliomleta kiziwi. Walitumia fursa vizuri na Yesu kumuomba amponye mwenzao. Kwa kuwa ni maongezi, walitumia ndimi zao vizuri. Na kwa sababu walitumia ndimi zao vizuri, Yesu alimponya yule kiziwi. Upo ujumbe wa kila mmoja kutumia ulimi wake kwa utukufu wa Mungu.
Baada ya uponyaji, wale waliomleta kiziwi kwa Yesu walienda kutangaza habari za Yesu. Walitangaza mambo aliyoyatenda. Yaani walitumia ulimi kumtangaza Kristo. Utumie ulimi wako kunena vema ili Mungu atukuzwe kupitia wewe. Ujumbe ni ule ule, kuwa na matumizi mazuri ya ulimi, kwa Utukufu wa Mungu. Ulimi usipotumika vizuri waweza kusababisha uovu.
Akihubiri juu ya somo hili, Siku moja katika mwaka wa 1533 BK, Mchg. Dkt. Martin Luther alisema;
"..Yesu anaonyesha kuwa anafungua masikio na ndimi zetu. Anatafuta kufanya hivi ndani ya Kanisa...Ni ukweli wa kibinadamu kuwa Mungu anatoa masikio yanayosikia na ndimi kwa wenye mwili, lakini kwa waaminio ni ukweli kiroho, kwamba anafungua masikio na kuponya ndimi zetu. Kwetu waaminio, lazima tulisikilize neno lake, na kutubu kwa midomo yetu"
"...Ni kweli kuwa tunaokolewa kwa kupitia neno la Mungu tu. Tujue nini tena kuhusu Mungu, kuhusu Bwana Yesu Kristo, sadaka yake, na Roho Mtakatifu? Leo ishara yake kuu na kazi ya pekee ni kutupa masikio ya neno lake, na ulimi wa kumheshimu, usiokufuru"
"...Watu wengi wako vibaya zaidi mara elfu kuliko kiziwi na bubu huyu, wana masikio yasiyofanya kazi. Wanalisikiliza neno la Mungu  lakini kwa uhalisia hawasikii na wala hawataki kusikia. Lakini wale wanaolisikia neno la Mungu, kwa furaha kabisa, ambao Kristo anawaambia Efata! (Funguka) wanao msaada....Kristo ametuonyesha njia ya kuingia ufalme wake kupitia neno lake, Injili Takatifu"
"...Mungu  anafungua ndimi zetu na anatuwezesha kuongea  kwa Imani, katika Kristo tunapata msamaha wa dhambi. Toba ni lazima. Tusiwe kimya, tuongee tuyaaminiyo mioyoni mwetu"
"...Ndimi zetu zikiwa sawa, masikio yakafunguka, Imani yetu inaanzia hapo, tukihubiri neno na Sakramenti. Wachungaji na wahubiri wengineo ni vidole vya Mungu wetu, kupitia kwao anatufungua ndimi na masikio yetu. Tukiwasikiliza, Mungu anaongea na mioyo yetu, kama kiziwi tuliyemsoma, Efata! Tunafunguliwa na tunakuwa siyo viziwi wala bubu tena"
"...Efata (funguka) Leo masikio yetu yanafunguliwa kuisikia habari njema ya Yesu Kristo, iliyoletwa kwetu kwa njia ya uponyaji wa kiziwi na bubu tuliyemsoma. Ujumbe ni kuwa, uponyaji wa mwili na roho ni zawadi ya Kristo kwetu. Ametusamehe kwa damu yake iliyomwagika msalabani. Atatufufua siku ya mwisho. Hii ndiyo Imani yetu, tumaini, linalosababisha ndimi zetu kuimba Utukufu"

(Martin Luther, 1533)

Uwe na siku njema