Jumapili ya tarehe 19.07.2026;
Siku ya Bwana ya 7 baada ya Utatu;
Masomo;
Zab 21:6-13
Mt 8:1-4
*Kut 33:12-17
Kutoka 33:12-17
12 Musa akamwambia Bwana, Angalia, wewe waniambia, Wachukue watu hawa; nawe hukunijulisha ni nani utakayemtuma pamoja nami. Walakini umesema, Nakujua jina lako, nawe umepata neema mbele zangu.
13 Basi, sasa nakuomba, ikiwa nimepata neema mbele zako, unionyeshe njia zako, nipate kukujua, ili nipate neema mbele zako; ukakumbuke ya kuwa taifa hilo ndilo watu wako.
14 Akasema, Uso wangu utakwenda pamoja nawe, nami nitakupa raha.
15 Naye akamwambia, Uso wako usipokwenda pamoja nami, usituchukue kutoka hapa.
16 Kwa maana itajulikanaje kuwa nimepata neema mbele zako, mimi na watu wako? Siyo kwa sababu unakwenda pamoja nasi, hata mimi na watu wako tutengwe na watu wote walio juu ya uso wa nchi?
17 Bwana akamwambia Musa, Nitafanya na neno hili ulilolinena, kwa maana umepata neema mbele zangu, nami nakujua jina lako.
Neema ya Mungu yatosha;
Utangulizi;
Baada ya Musa kuwa amepewa amri na Bwana kwa ajili ya Taifa lake (sura ya 20) aliendelea kupewa maagizo na Bwana ya kuwapa Israeli. Maagizo haya yalihusu jinsi ambavyo Israeli wangeendelea kuishi wakimtegemea yeye, kumfanyia ibada, kutoa sadaka, na kumtegemea katika maisha yao yote. Mtiririko wa maagizo unaonekana kama ifuatavyo katika kitabu cha Kutoka;
- Amri kumi za Mungu (sura ya 20)
- Sheria kuhusu watumwa (sura ya 21)
- Sheria za malipizo (Sura ya 22)
- Haki kwa wote (sura ya 23 na 24)
- Matoleo na sanduku la Agano (sura ya 25)
- Hema ya kukutania (sura ya 26)
- Madhabahu na sadaka za kuteketezwa (sura ya 27)
- Mavazi ya ukuhani na wakfu wao (sura ya 28 na 29)
- Madhabahu na kufukiza uvumba (sura ya 30)
- Sheria za sabato (sura ya 31)
- Sanamu ya ndama ya dhahabu (sura ya 32)
Inapofika sura ya 33 Bwana anampa Musa agizo la kuondoka Sinai. Anamtuma kuwaambia Israeli sasa waelekee Misri, nchi ambayo Bwana alimwapia Ibrahimu, Isaka na Yakobo. Bwana aliendelea kumwambia Musa kwamba Israeli walikuwa na roho ngumu, lakini akaendelea kuwaita wamsikie yeye. Wakaingia hemani, nguzo ya wingu ikashuka na kusimama mlangoni, watu wote wakasujudu mlangoni pa hema. Bwana akasema na Musa uso kwa uso kama mtu asemavyo na rafiki yake. Hadi hapa, nilikuwa najaribu kukuleta somo la leo linapoanzia.
Somo lenyewe;
Ni mazungumzo kati ya Mungu na Musa, Musa anamuomba Mungu kumuhakikishia kama iwapo angeendelea kuwaongoza wana wa Israeli hadi kuifikia nchi ya ahadi. Musa anakiri kumsikia Mungu akimwambia kuwa amepata neema ya kuwaongoza Israeli kuelekea Kanani. Anaendelea kumuomba Mungu kwamba kama amempa neema, basi amuoneshe njia zake apate kumjua. Zaidi Musa anaomba Mungu alikumbuke Taifa lake. Hapa Musa anaomba neema ya Mungu isiondoke kwa Israeli 12-13)
Katika kuendelea kuonesha kwamba Mungu asingewaacha Israeli, anampa jibu Musa ambalo ni miongoni mwa nukuu maarufu kwenye maandiko, pale Bwana aliposema "..uso wangu utakwenda pamoja nawe, nami nitakupa raha (14). Musa hakutaka kamwe Bwana awe mbali naye, itikio lake likawa "uso wako usipokwenda nami, usituchukue kutoka hapa" (15). Yaani Mungu amekwisha muelekeza Musa kutoka Sinai, lakini bado Musa anaongea na Bwana akionesha kumuhitaji katika kazi aliyomuita kuifanya, yaani kuwaongoza Israeli kuelekea nchi ya ahadi.
Musa anaendelea kuwa mdadisi, anamuuliza Bwana kwamba atajuaje kuwa amepata neema mbele zake, yeye na watu wa Mungu aliopewa kuwaongoza. Bwana anamtaka Musa kuwa na uhakika kwamba anayo neema mbele zake, anamjua jina lake (16-17). Bila shaka hadi hapa Musa aliiona neema ya Mungu juu yake, akaridhika na alichokiomba, yaani neema. Sasa akaomba utukufu wa Mungu! Mungu akamjibu kuwa Utukufu wake ni mkuu. Hebu soma hapa chini;
Kutoka 33:18-20
18 Akasema, Nakusihi unionyeshe utukufu wako.
19 Akasema, Nitapitisha wema wangu wote mbele yako, nami nitalitangaza jina la Bwana mbele yako; nami nitamfadhili yeye nitakayemfadhili; nitamrehemu yeye nitakayemrehemu.
20 Kisha akasema, Huwezi kuniona uso wangu, maana mwanadamu hataniona akaishi.
Neema ya Mungu yatosha;
Leo tunamuona Musa akiomba neema ya Mungu katika safari ya kuwaongoza wana wa Israeli kuelekea nchi ya ahadi. Iko wazi kwamba aliamini kwamba bila neema ya Mungu asingeweza! Katika kumjibu, Mungu hakujibu tu, bali katika kujibu aliitaja "neema" pia. Neno "neema" katika somo la leo linatokea mara tano (mistari 6). Waweza kuona ni vipi neema ilikuwa muhimu kwa Musa, na Israeli kwa ujumla.
Ni kwa neema hiyo hiyo Paulo anasema tumeokolewa;
Waefeso 2:8-10
8 Kwa maana mmeokolewa kwa neema, kwa njia ya imani; ambayo hiyo haikutokana na nafsi zenu, ni kipawa cha Mungu;
9 wala si kwa matendo, mtu awaye yote asije akajisifu.
10 Maana tu kazi yake, tuliumbwa katika Kristo Yesu, tutende matendo mema, ambayo tokea awali Mungu aliyatengeneza ili tuenende nayo.
Kwa neema ya Mungu tumeokolewa, hivyo tunahiitaji neema hiyo hiyo kuishi maisha ya wokovu utokao kwa Mungu pekee. Musa aliomba neema ya Mungu, na Mungu akaahidi neema kutopungua kwake. Itukumbushe kuwa bila neema ya Mungu hatuwezi lolote. Basi tuombe kila mmoja tudumu katika neema hii ya wokovu, ili sote kwa njia ya wokovu tulioupata kwa neema tuurithi uzima wa milele. Amina
Ibada njema
Heri Buberwa Nteboya
0784 968650
