Mwanzo 13:1-2 - 18-07-2026

Date
Reading
Mwanzo 13:1-2

Jumamosi asubuhi tarehe 18.07.2026;

Mwanzo 13:1-12

[1]Abramu akapanda kutoka Misri, yeye, na mkewe, na kila alichokuwa nacho, na Lutu pamoja naye, mpaka kusini.

[2]Naye Abramu alikuwa ni tajiri sana kwa mifugo, kwa fedha, na kwa dhahabu.

[3]Akaendelea kusafiri kutoka kusini mpaka Betheli, mahali pale palipokuwapo hema yake kwanza kati ya Betheli na Ai;

[4]napo ndipo palipokuwa na madhabahu aliyofanya hapo kwanza; naye Abramu akaliitia jina la BWANA hapo.

[5]Na Lutu aliyesafiri pamoja na Abramu, yeye naye alikuwa na makundi ya ng’ombe na kondoo, na hema.

[6]Na ile nchi haikuwatosha, ili wakae pamoja; maana mali zao zilikuwa nyingi, hata wasiweze kukaa pamoja.

[7]Kukawako ugomvi kati ya wachunga wanyama wa Abramu, na wachunga wanyama wa Lutu; na siku zile Wakanaani na Waperizi walikuwa wakikaa katika nchi.

[8]Abramu akamwambia Lutu, Basi, usiwepo ugomvi, nakusihi, kati ya mimi na wewe, wala kati ya wachungaji wangu na wachungaji wako; maana sisi tu ndugu.

[9]Je! Nchi hii yote haiko mbele yako? Basi ujitenge nami, nakusihi; ukienda upande wa kushoto, nitakwenda upande wa kuume; ukienda upande wa kuume, nitakwenda upande wa kushoto.

[10]Lutu akainua macho yake, akaliona Bonde lote la Yordani, ya kwamba lote pia lina maji, kabla BWANA hajaharibu Sodoma na Gomora, lilikuwa kama bustani ya BWANA, kama nchi ya Misri hapo unapokwenda Soari.

[11]Basi Lutu akajichagulia Bonde lote la Yordani; Lutu akasafiri kwenda upande wa mashariki; wakatengana wao kwa wao.

[12]Abramu akakaa katika nchi ya Kanaani, na Lutu akakaa katika miji ya lile Bonde; akajongeza hema yake mpaka Sodoma.

Upendo wa Mungu na utawale;

Asubuhi hii tunaona Abramu na  Lutu wakiwa eneo moja, lakini walikuwa na mifugo mingi sana kiasi kwamba eneo la  malisho halikutosha. Ilifikia hatua wachungaji wa mifugo yao walianza kugombana.

Abramu anakuwa mtu wa suluhu. Anamwambia Lutu kuwa hakuna haja ya kugombana, wakati malisho yako mengi. Lutu anapatana na wazo la Abramu, wanatengana, kila mtu anapata eneo la kutosha kulisha mifugo yake peke yake. Wanaopendana hawagombani. Tunawajibika kuishi maisha ya kupatana, na siyo kugombana, sisi kama Kanisa la Mungu tunaoiishi amri ya Upendo.

Ya nini kugombana?

Siku njema

Heri Buberwa Nteboya