Jumatano asubuhi 12.08.2026;
Mathayo 5:14-16
14 Ninyi ni nuru ya ulimwengu. Mji hauwezi kusitirika ukiwa juu ya mlima.
15 Wala watu hawawashi taa na kuiweka chini ya pishi, bali juu ya kiango; nayo yawaangaza wote waliomo nyumbani.
16 Vivyo hivyo nuru yenu na iangaze mbele ya watu, wapate kuyaona matendo yenu mema, wamtukuze Baba yenu aliye mbinguni.
Haki huleta amani na ustawi;
Yesu yuko mlimani anafundisha, sehemu tuliyoisoma anawaambia umati waliomsikiliza kwamba wao ni nuru ya ulimwengu. Anawaambia kwamba taa huwekwa mahali ambapo itawaangazia wote waliomo ndani waone. Vivyo hivyo anawataka wasikilizaji wake kuwa nuru, waangaze mbele za watu matendo yao yaonekane ili Baba aliye mbinguni atukuzwe.
Tunakumbushwa kuwa sisi nasi ni nuru ya ulimwengu. Tunatumwa kuwaangazia wengine wamjue Yesu Kristo na kumpokea. Maisha yetu yawe nuru, yaani tuishi maisha ya ushuhuda, tuangaze. Tukiwa nuru ya ulimwengu yote tufanyayo yanakuwa kwa utukufu wa Mungu. Amina
Siku njema
Heri Buberwa
Butainamwa/Bukoba
