Jumatatu asubuhi tarehe 24.08.2026;
Hesabu 14:1-10
1 Mkutano wote wakapaza sauti zao wakalia; watu wakatoka machozi usiku ule.
2 Kisha wana wa Israeli wote wakamnung'unikia Musa na Haruni; mkutano wote wakawaambia, Ingekuwa heri kama tungalikufa katika nchi ya Misri, au, ingekuwa heri kama tungalikufa katika jangwa hili.
3 Mbona Bwana anatuleta mpaka nchi hii ili tuanguke kwa upanga? Wake zetu na watoto wetu watakuwa mateka; je! Si afadhali turudi Misri?
4 Wakaambiana, Na tumweke mtu mmoja awe akida, tukarudi Misri.
5 Ndipo Musa na Haruni wakaanguka kifudifudi mbele ya mkutano wa kusanyiko la wana wa Israeli.
6 Na Yoshua mwana wa Nuni, na Kalebu mwana wa Yefune, waliokuwa miongoni mwao walioipeleleza nchi, wakararua nguo zao;
7 wakanena na mkutano wote wa wana wa Israeli wakasema, Nchi ile tuliyopita kati yake ili kuipeleleza, ni nchi njema mno ya ajabu.
8 Ikiwa Bwana anatufurahia, atatuingiza katika nchi hii atupe iwe yetu, nayo ni nchi yenye wingi wa maziwa na asali.
9 Lakini msimwasi Bwana, wala msiwaogope wale wenyeji wa nchi, maana wao ni chakula kwetu; uvuli uliokuwa juu yao umeondolewa, naye Bwana yu pamoja nasi; msiwaogope.
10 Lakini mkutano wote wakaamuru wapigwe kwa mawe. Ndipo utukufu wa Bwana ukaonekana katika hema ya kukutania, mbele ya wana wa Israeli wote.
Tutumie ndimi zetu kwa Utukufu wa Mungu;
Baada ya Musa kuwa amewatuma watu kuipeleleza nchi ya ahadi, walirudi na ripoti ambayo haikuwafurahisha Israeli. Ngoja nikuoneshe sehemu kidogo inayoonesha hilo;
Hesabu 13:31-33
31 Bali wale watu waliopanda pamoja naye wakasema, Hatuwezi kupanda tupigane na watu hawa; kwa maana wana nguvu kuliko sisi.
32 Wakawaletea wana wa Israeli habari mbaya ya ile nchi waliyoipeleleza, wakasema, Ile nchi tuliyopita kati yake ili kuipeleleza, ni nchi inayowala watu wanaoikaa; na watu wote tuliowaona ndani yake ni watu warefu mno.
33 Kisha, huko tuliwaona Wanefili, wana wa Anaki, waliotoka kwa hao Wanefili; tukajiona nafsi zetu kuwa kama mapanzi; nao ndivyo walivyotuona sisi.
Somo la asubuhi hii linaanzia hapo, Israeli wanalia na kutokwa machozi, wanatamani kurudi Misri! Wanamwambia Musa kuwa bora wangelikufa Misri au jangwani! Musa, Haruni, na wale waliotumwa kuipeleleza nchi ya ahadi wakawaangukia Israeli kuwasihi wasimwasi Bwana, lakini umati ukaamuru kutaka wapigwe mawe! Kwa hiyo ni habari ya uasi wa Israel baada ya kupokea habari mbaya kuhusu Kanaani.
Tunajifunza nini?
1. Kuangalia matatizo badala ya Mungu anayetuwezesha kunaweza kusababisha kutosa utii kwa Mungu.
2. Mungu anapotusamehe dhambi, haimaanishi changamoto za kila siku kukosekana katika maisha yetu, bali kwa msaada wake tunaweza kuzikabili.
3. Musa aliwaombea toba Israeli, akasimama kama mpatanishi wa Israeli kwa Mungu na kuwaombea. Anakuwa alama ya uongozi bora na upendo ambayo ni amri kuu.
4. Musa, Yoshua, Kalebu na wapelelezi hawakuvutwa na nguvu ya umma kutaka kumwasi Bwana na kurudi Misri, bali walisimama kumtii Bwana kuelekea Kanaani. Simama kwa nafasi yako ukiitetea kweli ya Mungu.
5. Israeli walitumia ndimi zao vibaya kutaka kukataa maelekezo toka kwa Mungu pale walipojadiliana na kutaka kurudi Misri. Tumia ulimi wako kwa Utukufu wa Mungu. Amina
Tunakutakia wiki njema yenye matumizi bora ya ulimi.
Heri Buberwa Nteboya
0784 968650
