Alhamisi asubuhi tarehe 23.07.2026;
Zaburi 107:33-43
33 Amegeuza mito ikawa jangwa, Na chemchemi za maji zikawa nchi ya kiu.
34 Nchi ya matunda mengi ikawa uwanda wa chumvi, Kwa sababu ya ubaya wao walioikaa.
35 Amegeuza jangwa ikawa ziwa la maji, Na nchi kavu ikawa chemchemi za maji.
36 Maana amewakalisha huko wenye njaa, Nao wametengeneza mji wa kukaa.
37 Wakapanda mbegu katika mashamba, Na kutia mizabibu iliyotoa matunda yake.
38 Naye huwabariki wakaongezeka sana, Wala hayapunguzi makundi yao.
39 Kisha wakapungua na kudhilika, Kwa kuonewa na mabaya na huzuni.
40 Akawamwagia wakuu dharau, Na kuwazungusha katika nyika isiyo na njia.
41 Akamweka mhitaji juu mbali na mateso, Akamfanyia jamaa kama kundi la kondoo.
42 Wanyofu wa moyo wataona na kufurahi, Na uovu wa kila namna utajifumba kinywa.
43 Aliye na hekima na ayaangalie hayo; Na wazitafakari fadhili za Bwana.
Neema ya Mungu yatosha;
Zaburi ya 107 inahusu upendo wa Mungu usiokoma, na utayari wa Mungu kuwaokoa watu wake na shida zao wakati wote. Zaburi inaonesha ukuu wa Mungu kwa kugeuza mito kuwa jangwa, chemchemi za maji zikawa nchi ya kiu, jangwa likawa ziwa la maji n.k Bwana amewabariki wenye njaa, akamfariji mhitaji na kumpa atakayo, fadhili zake ni za milele.
Sasa ukiangalia tulivyoandika hapo juu, ni matendo makuu ya Mungu kama Zaburi inavyosomeka. Pamoja na ukuu wa Mungu kuonekana, yote hayo ni neema yake kwa watu wake. Ni kwa neema hiyo anatutendea nasi makuu kila siku katika maisha yetu. Tusimuache Kristo mwenye neema, ili atupe mwisho mwema. Amina
Alhamisi njema
Heri Buberwa
Mlutheri
