
Jumatatu asubuhi tarehe 19.10.2026;
Yeremia 17:19-27
19 Bwana akaniambia hivi, Enenda ukasimame katika lango la wana wa watu hawa, waingiapo wafalme wa Yuda, na watokeapo, na katika malango yote ya Yerusalemu,
20 ukawaambie, Lisikieni neno la Bwana, enyi wafalme wa Yuda, na Yuda wote, nanyi wenyeji wote wa Yerusalemu, ninyi mwingiao kwa malango haya;
21 Bwana asema hivi, Jihadharini nafsi zenu, msichukue mzigo wo wote siku ya sabato, wala msiulete ndani kwa malango ya Yerusalemu;
22 wala msitoe mzigo katika nyumba zenu siku ya sabato, wala msifanye kazi yo yote; bali itakaseni siku ya sabato, kama nilivyowaamuru baba zenu;
23 lakini hawakusikiliza, wala hawakutega masikio yao, bali walifanya shingo zao kuwa ngumu, ili wasisikilize wala wasipokee mafundisho.
24 Na itakuwa, kama mkinisikiliza mimi kwa bidii, asema Bwana, msiingize mzigo wo wote kwa malango ya mji huu siku ya sabato, bali mkiitakasa siku ya sabato, bila kufanya kazi yo yote siku hiyo;
25 ndipo watakapoingia wafalme na wakuu kwa malango ya mji huu; wataketi katika kiti cha enzi cha Daudi, na kupanda magari na farasi, wao, na wakuu wao, watu wa Yuda, na wenyeji wa Yerusalemu; na mji huu utakaa hata milele.
26 Nao watatoka miji ya Yuda, na mahali palipo pande zote za Yerusalemu, na nchi ya Benyamini, na Shefela, na milima,na upande wa Negebu,wakileta sadaka za kuteketezwa,na dhabihu,na sadaka za unga,na ubani,wakileta pia sadaka za shukurani,nyumbani kwa BWANA.
27 Lakini kama hamtaki kunisikiliza, kuitakasa siku ya sabato, kutokuchukua mzigo na kuingia kwa malango ya Yerusalemu siku ya sabato; basi, nitawasha moto malangoni mwake, nao utaziteketeza nyumba za enzi za Yerusalemu, wala hautazimika.
Madhara ya kudharau wito;
Bwana Asifiwe!
Somo la asubuhi ya leo ni ujumbe wa kinabii kutoka kwa Mungu kupitia kwa Nabii Yeremia kuhusu umuhimu wa kuitunza Sabato. Mungu alimwambia Yeremia kusimama kwenye lango la Yerusalemu mahali ambapo mfalme wa Yuda aliingilia na kutoka, na malango mengine ya mji. Mfalme na watu wake walikuwa wanapewa amri ya kutobeba mizigo, pia kutofanya kazi siku ya Sabato. Walitakiwa kuitakasa Sabato kama walivyoamriwa baba zao.
Kwa kutii amri ya kuitunza Sabato, Wafalme wanaahidiwa kuendelea kuingia mjini kwa farasi na magari, wao na watu wote katika Yuda na Yerusalemu yote. Lakini wasipotii, ahadi Bwana ni kuwasha moto kwenye malango ya Yerusalemu na kuziteketeza nyumba za enzi za Yerusalemu.
Somo linatufundisha nini?
1. Israeli walitakiwa kuishika Sabato kama alivyoamuru Bwana, yaani ilikuwa ni amri kwa sababu walitakiwa kumsikiliza na kumtii Bwana. Sisi leo tunakumbushwa kumtii Bwana kwa njia ya neno lake.
2. Tusiwe na mioyo migumu - pamoja na maonyo toka kwa Bwana, watu walifanya uovu wakakataa kumsikiliza Bwana, ikasababisha wapelekwe uhamishoni Babeli. Kutomwamini Yesu kuna mwisho 5g usio mzuri.
3. Israeli waliamriwa kuishika sabato. Leo Yesu Kristo ndiye Bwana wa Sabato, mwenye amri juu ya vitu vyote. Kumbe tumwamini Kristo ambaye ni Bwana wa Sabato, lakini anayo pia mamlaka ya kusamehe dhambi na kutupa uzima wa milele. Amina
Tunakutakia wiki njema
Heri Buberwa Nteboya
0784 968650
