
Jumatano asubuhi tarehe 07.10.2026
Wagalatia 3:7-14
7 Fahamuni basi, ya kuwa wale walio wa imani, hao ndio wana wa Ibrahimu.
8 Na andiko, kwa vile lilivyoona tangu zamani kwamba Mungu atawahesabia haki Mataifa kwa imani, lilimhubiri Ibrahimu habari njema zamani, kusema, Katika wewe Mataifa yote watabarikiwa.
9 Basi hao walio wa imani hubarikiwa pamoja na Ibrahimu aliyekuwa mwenye imani.
10 Kwa maana wale wote walio wa matendo ya sheria, wako chini ya laana; maana imeandikwa, Amelaaniwa kila mtu asiyedumu katika yote yaliyoandikwa katika kitabu cha torati, ayafanye.
11 Ni dhahiri ya kwamba hakuna mtu ahesabiwaye haki mbele za Mungu katika sheria; kwa sababu Mwenye haki ataishi kwa imani.
12 Na torati haikuja kwa imani, bali, Ayatendaye hayo ataishi katika hayo.
13 Kristo alitukomboa katika laana ya torati, kwa kuwa alifanywa laana kwa ajili yetu; maana imeandikwa, Amelaaniwa kila mtu aangikwaye juu ya mti;
14 ili kwamba baraka ya Ibrahimu iwafikilie Mataifa katika Yesu Kristo, tupate kupokea ahadi ya Roho kwa njia ya imani.
Uhuru wa Mkristo;
Mtume Paulo anawaandikia Wagalatia kuhusu sheria na imani, kwamba Mungu huwahesabia watu haki kwa imani. Anasema wote walio wa matendo ya sheria wako chini ya laana! Anakazia kwamba hakuna mtu ahesabiwaye haki mbele za Mungu katika sheria, kwa sababu mwenye haki ataishi kwa imani.
Msisitizo wa Paulo ni kwamba Kristo alitukomboa na laana ya torati (alishinda kifo) kwa kuwa alifanywa laana kwa ajili yetu, maana imeandikwa "Amelaaniwa kila mtu atungikwaye juu ya mti" Hapa Mtume Paulo alikuwa anairejea torari;
Kumbukumbu la Torati 21:22-23
22 Akiwa mtu ametenda dhambi ipasayo kufa, akauawa, nawe ukamtundika juu ya mti;
23 mzoga wake usikae usiku kucha juu ya mti; lazima utamzika siku iyo hiyo; kwani aliyetundikwa amelaaniwa na Mungu; usije ukatia unajisi katika nchi yako akupayo Bwana, Mungu wako, iwe urithi wako.
Kama Mtume Paulo anavyosema, kwamba Kristo alitukomboa na laana ya torati, tunapomwamini tunakuwa hatuko chini ya sheria, bali kwa neema yake tunaokolewa. Tuko huru kwa njia ya wokovu aliotupa Kristo bure kwa neema yake, hivyo tisitishwe na mafundisho ya sheria yaliyojaa vitisho. Neema ya Mungu yatosha. Amina
Siku njema
Heri Buberwa
