VIDEOS

Angalia picha mjongeo (Video) za ibada na matukio maalum ya Usharika hapa https://m.youtube.com/@AZANIAFRONTCATHEDRAL

Date
Reading
Wagalatia 3:23-29

Alhamisi asubuhi tarehe 08.10.2026;

Wagalatia 3:23-29

[23]Lakini kabla ya kuja ile imani tulikuwa tumewekwa chini ya sheria, tumefungwa mpaka ije ile imani itakayofunuliwa.

[24]Hivyo torati imekuwa kiongozi kutuleta kwa Kristo, ili tuhesabiwe haki kwa imani.

[25]Lakini, iwapo imani imekuja, hatupo tena chini ya kiongozi.

[26]Kwa kuwa ninyi nyote mmekuwa wana wa Mungu kwa njia ya imani katika Kristo Yesu.

[27]Maana ninyi nyote mliobatizwa katika Kristo mmemvaa Kristo.

[28]Hapana Myahudi wala Myunani. Hapana mtumwa wala huru. Hapana mtu mume wala mtu mke. Maana ninyi nyote mmekuwa mmoja katika Kristo Yesu.

[29]Na kama ninyi ni wa Kristo, basi, mmekuwa uzao wa Ibrahimu, na warithi sawasawa na ahadi.

Uhuru wa Mkristo;

Katika sura ya 3 ya waraka kwa Wagalatia, Mtume Paulo anafanya ufafanuzi wa wazi kuhusu kipaumbele cha ahadi ya Mungu kwa Ibrahimu na utimilifu wa ahadi hiyo katika Yesu Kristo, na nafasi ya sheria katikati ya ahadi ya Mungu. Somo tulilosoma kuanzia mstari wa 23 hadi 29 ni hitimisho la hoja ya Mtume Paulo, hivyo ni vizuri kuangalia hoja za Mtume Paulo kuanzia mwanzoni mwa sura ya 3 ili kupata sura ya somo;

Fuatana nasi;

Paulo alipata shida kwamba waamini  wa  Galatia walishawishika kukubali tohara na kuzingatia sheria za kiyahudi  kama vitu muhimu katika ahadi ya Mungu. Paulo anawakumbusha watu wa Galatia kuwa walimpokea Roho Mtakatifu kwa kuamini tangazo la Kristo aliyesulibiwa na siyo kwa kazi ya sheria (3:1-5). Katika nyaraka zake, Paulo anatumia neno "sheria" (Kiyunani "nomos") kurejea sheria ya Musa na vitabu vitano vya kwanza vya Biblia, yaani Torati.
Paulo  anaisoma Torati kama maelezo, ambapo Kristo ndiye mwenye maelezo ya mwisho. Kwa maana hiyo Torati inaelekezwa kwa Yesu maana ndiye mwenye maelekezo ya mwisho. Paulo anaiangalia sheria  torati kwa mtazamo mpya katika Kristo Yesu. Hivyo katika sura hii ya tatu Paulo anaigeuza torati kuwa maelezo kuweka ufafanuzi wake.

Kipaumbele cha ahadi;

Katika kitabu cha Mwanzo 15:6 baada ya Mungu kumuahidi Ibrahimu uzao kama nyota zilizoko mbinguni, Ibrahimu "alimwamini Mungu" na akafanyika mwenye haki. Katika Mwz 12:3 na 22:18 Mungu alimuahidi Ibrahimu kuwa katika yeye (Ibrahimu) jamaa zote za dunia watabarikiwa. Kwa maoni yangu Paulo anaangalia mistari hii kama ushahidi kwamba Mungu alipanga tokea mwanzo kuwahesabia watu wake haki kwa Imani. Kwangu mimi naona Bwana  alitangaza Injili kabla, kwa Ibrahimu, kwamba mwanadamu ataokolewa kwa Imani (Gal 3:6-9)
Katika mstari wa 10 hadi 20, Mtume Paulo anaonesha jinsi sheria ilivyowekwa na kazi yake;
-Sheria haiwezi kuleta baraka, hutangaza laana kwa asiyeishika. Kristo alitukomboa kutoka kwenye laana ya sheria alipokufa msalabani (3:10-14)
-Ahadi ya Mungu ina kipaumbele toka mwanzo, ilitolewa takribani miaka 430 kabla ya sheria ya Musa. Sheria haiwezi kuondoa ahadi asilia iliyopokelewa kwa Imani (3:15-18)
-Sheria ilitolewa na Musa kwa njia ya malaika wa Bwana, wakati ahadi ilitolewa na Mungu mwenyewe kwa Ibrahimu (3:19-20)
Somo lenyewe;
Hadi hapo Mtume Paulo anaonesha nafasi ya sheria na ahadi ya Mungu iliyopokelewa kwa Imani. Ndiyo maana anaanza kwenye somo la  asubuhi hii kusema kuwa kabla ya Imani, tulikuwa katika kifungo cha sheria hadi Imani ilipodhihirika. Sheria ilikuwa kipimo hadi Kristo alipokuja, ili tuhesabiwe haki kwa Imani. Hadi hapo naweza kusema kuwa, Mtume Paulo anatukumbusha kuwa tunahesabiwa haki kwa Imani. Sisi sote ni watoto wa Mungu kama tulivyompokea kwa imani (25-26)
Mstari wa 27  ni uthibitisho kuwa sote tumebatizwa katika Kristo, na kwa njia hiyo tumemvaa Kristo. Wote waliobatizwa katika Kristo ni washirika wake, na yeye ndiye Mwokozi wao. Mtume Paulo anawaambia Wagalatia kuwa kama wao ni wafuasi wa Kristo, basi wamekuwa uzao wa Ibrahimu, na warithi sawasawa na ahadi. Kumbe kila amwaminiye Kristo anayo ahadi ya Baba. 
Katika kumfuata Kristo kwa Imani ya kweli, Paulo anasema hakuna tena Myahudi wala Myunani, mtumwa wala huru, mume wala mke. Maana yake ni kwamba Yesu hachagui wa kumuokoa, huwaokoa wote. Wokovu aliouleta ni kwa ajili ya wote. Hadi hatua hii tusisahau kuwa wokovu huu ni kwa njia ya Imani. Kumbe tunapomwamini Yesu tunakuwa wana wa Mungu, hivyo tudumu katika yeye ili tuwe huru, pia kuwa na mwisho mwema. Amina

Siku njema

Heri Buberwa