Date
Reading
Ufunuo wa Yohana 14:13

Jumamosi asubuhi tarehe 07.11.2026;
Ufunuo wa Yohana 14:13
[13]Nikasikia sauti kutoka mbinguni ikisema, Andika, Heri wafu wafao katika Bwana tangu sasa. Naam, asema Roho, wapate kupumzika baada ya taabu zao; kwa kuwa matendo yao yafuatana nao.
Tunaitwa kuwa wenyeji wa Mbinguni;
Katika elimu ya Theologia ya Agano la kale, hakuna maandiko ya moja kwa moja kuhusu uzima wa milele, na ufufuo wa wafu. Lakini ukiangalia manabii na watakatifu wengineo walivyokuwa wakiomba na kumsihi Mungu kama mkuu akaaye juu ya vyote, utakubali kuwa walikiri maisha yajayo baada ya yale waliyoishi, maisha ambayo Bwana Yesu mwenyewe alikuja kutuandaa kwa ajili ya kuyaendea. Hivyo katika kazi yake, pamoja na mengine yote, Bwana Yesu alikuja kutuandaa kwa ajili ya uzima baada ya maisha haya.
Bwana Yesu anatukumbusha kuwa;
Siku moja sisi sote tutakuwa katika ulimwengu mwingine. Lengo la somo la leo ni kujifunza kuwa tunaweza kujiandaa vipi kuuelekea huo ulimwengu mwingine. Kila mtu anayeishi hufa katika njia mbili;
Yohana 8:24
[24]Kwa hiyo naliwaambieni ya kwamba mtakufa katika dhambi zenu; kwa sababu msiposadiki ya kuwa mimi ndiye, mtakufa katika dhambi zenu.
Kuna kufa katika Kristo, na kufa katika dhambi zetu. Sasa asubuhi ya leo tunauangalia mstari tuliousoma, ambao mkazo wake ni "Heri wafu wafao katika Bwana..." Tunapoishi duniani, ni lazima tutakufa katika Bwana, au katika dhambi. Kufa katika dhambi ni kubeba dhambi zako hadi kifo. Unaondoka duniani kwa njia ya kifo, lakini Mungu yupo! Unaondoka na dhambi zako! Halafu unasimama mbele za Mungu na dhambi zako. Ni jambo la kutisha sana! Lakini ipo njia nyingine ya kufa. Kama tulivyosoma, "Heri wafu wafao katika Bwana....." Bwana Yesu alizichukua dhambi zetu alipokufa, ili kama tuko kwake, tusiwe nazo.
Kufa katika Bwana kwa toba, ni ahadi yetu sote tunaoamini. Ahadi haimaanishi ni maisha mepesi kuelekea kifo hicho. Inatuelekeza kutochoka katika maisha ya ufuasi. Ni muhimu kuishi ukristo wa gharama, kitu ambacho wengi waliomwamini na kumfuata Bwana Yesu walifanya, na hata ilipobidi walikufa kifo kibaya, kama Yohana Mbatizaji
Kwa nini tuna Heri tukifa katika Bwana?
a)Tunapumzika kazi ngumu.
Ukristo siyo swala la kufanya jambo fulani tu kwa sababu ni mkristo, ukristo ni kujitoa kweli katika kumfuata Kristo. Kusema tu mimi ni mkristo hakunifanyi kuwa mkristo, bali kuuishi ukristo, ambao msingi wake ni neno la Mungu.
Kumtumikia Mungu siyo kazi rahisi. Unahitajika kujitoa kweli kweli. Tunamtumikia Mungu duniani, ambapo tukifa tutapumzika kazi za duniani, na kwenda kuanza kazi mbinguni. Ni muhimu kujua kuwa ukijitoa kumtumikia Mungu, kuna kukutana na ugumu katika kazi yenyewe, kukatishwa tamaa, kuchoka n.k Lakini mbinguni ni tofauti, mambo ya namna hiyo hayapo.
Zipo kazi ambazo zinafanyika hapa duniani tu. Yaani anayefanya akimaliza anapumzika. Wapo ambao wakifa katika Bwana watakuwa wamemaliza. Kwa mtazamo wa Injili, mfano, wachungaji watakuwa wa kwanza kuwa nje ya kazi mbinguni. Ni ajabu?
Tutahitaji mahubiri wakati tuko mbinguni tayari? Tutahitaji ushauri wakati tayari tumefika? Tutahitaji vipi kutunzwa kichungaji wakati tumeshafika kwa Mchungaji mkuu, na tumekwisha kufutwa machozi?
Kazi unayoifanya inaweza kuonekana kubwa, wakati mwingine kukata tamaa. Kule mbinguni hiyo kazi haitakuwepo. Sote tutakuwa tukimtumikia Bwana Yesu kwa nguvu mpya na furaha ya milele. Hautafanya kazi mbinguni, hivyo nafasi yako ya pekee ni kutumika sasa hivi.
Sala utakazoomba ni sala uombazo sasa
Injili utakayohubiri ni Injili uhubiriyo sasa
Ushindi wa dhambi ujao, ni ule ulio nao sasa
Watoto utakaowafundisha, ni wale uwafundishao sasa
Matoleo yako ya baadae, ni matoleo yako ya sasa
Kusimama kwako siku ile, kunategemea umesimamaje sasa
Namaanisha nini?
Fanya kazi kwa bidii, juhudi na maarifa, kwa Utukufu wa Mungu, ili kazi zako zikutetee mbele za Mungu.
Kutakuwa na furaha ya milele katika Kristo, lakini tunao muda mfupi ma kuandaa mazingira ya furaha hiyo. Tumia fursa kutimiza wajibu wako kuelekea mwisho mwema.
b) Matendo yetu yanatufuata;
Wakristo wakiingia mbinguni, matendo yao yanakuwa nyuma yao, na siyo mbele. Mkristo haiingii mbinguni kwa sababu ya matendo yake, "matendo yanamfuata"
Bwana Yesu alisema;
Yohana 14:2
[2]Nyumbani mwa Baba yangu mna makao mengi; kama sivyo, ningaliwaambia; maana naenda kuwaandalia mahali.
Bwana Yesu ndiye mwanzilishi wa Imani yetu. Anatangulia kwanza kufungulia milango ya mbingu, na wale wanaomfuata wanaingia, na matendo yao yanawafuata. Matendo mema yanaongoza njia ya kwenda mbinguni. Tunapodumu katoka toba ya kweli na msamaha, Yesu anaahidi kutusafisha dhambi zetu. Katika maisha yetu ya Sala, tusisahau toba ya kweli iletayo ondoleo la dhambi, ili matendo yetu yatufikishe kwenye uzima wa ulimwengu ujao.
c) Tunakufa katika Bwana;
Sio wote wafao wamebarikiwa, wengine wanakufa dhambini. Mbingu inamtambua aliyekufa katika Imani. Mbingu inamtambua aliyekufa katika Beana kwa sababu wanakufa katika Imani. Bwana Yesu alifundisha hili alipotoa mfano wa tajiri na Lazaro;
Luka 16:22
[22]Ikawa yule maskini alikufa, akachukuliwa na malaika mpaka kifuani kwa Ibrahimu. Yule tajiri naye akafa, akazikwa.
Yule tajiri aliishia kuzikwa tu, lakini yule maskini hakuishia kuzikwa tu, aliingia mbinguni. Alikufa katika Bwana.
Tunawajibika kuishi katika Imani ili tufe katika Bwana.
Tunapoiendea mbingu;
Wakati mwingine tunakumbana na udhaifu katika mwenendo wetu wa kila siku, lakini matendo yetu yako nyuma yetu. Tusiangalie maisha tuliyoishi kwa ajili ya Kristo, bali maisha aliyoishi kwa ajili yetu. Tusahau yote na kukumbuka Yesu alivyotufia msalabani.
Tusiangalie tumefanya nini, au tumeshindwa nini, tumwangalie Kristo. Kuingia mbinguni hakuji kwa tulichomfanyia Krsto, bali kwa alichotufanyia. Tukitambua ujio na kazi yake, tunatimiza wajibu wetu tukiongozwa na neno lake, ili kuifikia mbingu tuliyoahidiwa. Hii ndiyo habari njema tunayoihitaji tunapoishi, na hata kufa.
Tunapomaliza mwaka wa Kanisa, tunakumbushwa kuwa upo mwisho wa dunia. Yesu atarudi. Tutafakari, tunajiandaaje kuufikia mwisho huo? Masadukayo hawakuamini katika ufufuo! Sasa siku wakisimama hukumuni sijui watajibuje? Tafakari njia zako kuelekea kuwa Mwenyeji wa mbinguni
Jumamosi njema
Heri Buberwa Nteboya
0784 968650
