PICHA: Maendeleo ya Ujenzi wa Nyumba za Wageni, Kituo cha Kiroho Kiharaka

Mchungaji Kiongozi wa Usharika wa Kanisa Kuu Azania Front, Chaplain Victor Makundi amewashukuru washarika kwa kuendelea kutoa michango yao ili kukamilisha ujenzi wa nyumba za wageni unaoendelea katika Kituo cha Kiroho Kiharaka, Bagamoyo mkoani Pwani.

Akitoa tathimini na mwelekeo wa ujenzi wa nyumba hizo katika ibada ya Jumapili, 2 Agosti 2026, Usharikani Azania Front, Chaplain Makundi amesema mradi huo unatarajiwa kukamilika mwaka 2028, hivyo amewaomba washarika kuendelea kutoa michango yao ili lengo la kukamilisha mradi huo kwa wakati liweze kutimia.

"Nawashukru wote kwa michango yenu, fedha na mali mnazozitoa. Sisi bado tuko site usiku na mchana, kazi zinafanyika na hakuna kulala," alisema Chaplain Makundi.

"Pia, nawakaribisha wakristo, bado nafasi zipo,  nyumba bado zipo chache, tutoe michango yetu kwa moyo tukijua kwamba kazi hii inatuhusu sisi sote," aliongeza.

Angalia hizi picha za drone zikionyesha hatua iliyofikiwa katika ujenzi wa nyumba za wageni unaoendelea katika kituo cha Kiroho Kiharaka (Julai 2026).