Matendo ya mitume 6:1-7 - 31-07-2026

Date
Reading
Matendo ya mitume 6:1-7

Ijumaa asubuhi tarehe 31.07.2026

Matendo ya Mitume 6:1-7

1 Hata siku zile wanafunzi walipokuwa wakiongezeka hesabu yao, palikuwa na manung'uniko ya Wayahudi wa Kiyunani juu ya Waebrania kwa sababu wajane wao walisahauliwa katika huduma ya kila siku.

2 Wale Thenashara wakawaita jamii ya wanafunzi, wakasema, Haipendezi sisi kuliacha neno la Mungu na kuhudumu mezani.

3 Basi ndugu, chagueni watu saba miongoni mwenu, walioshuhudiwa kuwa wema, wenye kujawa na Roho, na hekima, ili tuwaweke juu ya jambo hili;

4 na sisi tutadumu katika kuomba na kulihudumia lile Neno.

5 Neno hili likapendeza machoni pa mkutano wote; wakamchagua Stefano, mtu aliyejaa imani na Roho Mtakatifu, na Filipo, na Prokoro, na Nikanori, na Timoni, na Parmena, na Nikolao mwongofu wa Antiokia;

6 ambao wakawaweka mbele ya mitume, na walipokwisha kuomba wakaweka mikono yao juu yao.

7 Neno la Mungu likaenea; na hesabu ya wanafunzi ikazidi sana katika Yerusalemu; jamii kubwa ya makuhani wakaitii ile Imani.

Mungu hupendezwa na moyo wa toba;

Wakati Mitume wanaianza huduma yao upo wakati  wajane wa Wayahudi wa Kiyunani walisahauliwa katika huduma ya kila siku. Mitume walipoliona jambo hili, wakaona washirikishe jamii nzima ya Kanisa. Kanisa likaunda kamati ya watu saba ili kulisimamia jambo hilo ili Mitume waendelee na kazi yao. Kamati hiyo iliongozwa na Stefano. Kwa usimamizi mzuri wa kamati, Mitume waliendelea na huduma, na Kanisa likaendelea kukua katika Yerusalemu.

Mitume walitambua kosa kuwepo, na katika kulitatua wakaona kwamba peke yao wasingeweza. Walilitatua kwa kuwashirikisha waumini wote. Tunapoitenda kazi ya Mungu kwa pamoja, tushirikishane vipawa vyetu, maana kila mtu akitumia kipawa chake na kutimiza wake, huduma ya Kanisa inaimarika. Kanisa ni la Mungu kwa ajili ya wote. Kila mmoja atumike kwa karama na nafasi yake.  Viongozi wa Kanisa acheni kuzima wito wa waamini, mtawajibika mbele za Mungu. Tubuni sasa na mruhusuni kila mmoja kutumika kwa kadri ya wito na kipawa chake. Amina

Siku njema

Heri Buberwa