Luka 19:1-9 - 26-07-2026

Date
Reading
Luka 19:1-9

Jumapili ya tarehe 26.07.2026;

Siku ya Bwana ya 8 baada ya Utatu;

Masomo;

Zab 51:11-14

Ebr 12:5-11

*Luka 19:1-9

Luka 19:1-9

1 Naye alipoingia Yeriko alipita katikati yake.

2 Na tazama, palikuwa na mtu, jina lake Zakayo, mkubwa mmoja katika watoza ushuru, naye ni tajiri.

3 Huyu alikuwa akitafuta kumwona Yesu ni mtu wa namna gani, asiweze kwa sababu ya umati wa watu, maana ni mfupi wa kimo.

4 Akatangulia mbio, akapanda juu ya mkuyu apate kumwona, kwa kuwa atakuja kuipitia njia ile.

5 Na Yesu, alipofika mahali pale, alitazama juu, akamwambia, Zakayo, shuka upesi, kwa kuwa leo imenipasa kushinda nyumbani mwako.

6 Akafanya haraka, akashuka, akamkaribisha kwa furaha.

7 Hata watu walipoona, walinung'unika wote, wakisema, Ameingia kukaa kwa mtu mwenye dhambi.

8 Zakayo akasimama, akamwambia Bwana, Tazama, Bwana, nusu ya mali yangu nawapa maskini, na ikiwa nimenyang'anya mtu kitu kwa hila namrudishia mara nne.

9 Yesu akamwambia, Leo wokovu umefika nyumbani humu, kwa sababu huyu naye ni mwana wa Ibrahimu.

Mungu hupendezwa na moyo wa toba;

Kanisa la kwanza, na hata baada ya mgawanyiko (Eastern Orthodox & Greek Catholic) katika utaratibu wa Liturjia, lilitumia somo la Zakayo kwenye juma la mwisho kabla ya majira ya mateso (Lent). Lengo haswa ilikuwa ni mambo mawili. Kwanza, Yesu kumuita Zakayo kushuka mtini ilikuwa ni ishara ya Yesu kuwaita watu kutubu. Pili, tendo la Zakayo kutubu lilitumika kuwahimiza waamini kutubu. Kanisa lilitumia somo la Zakayo kuwaanda watu kwa ajili ya majira ya mateso, likiwakumbusha juu ya toba iletayo wokovu. Hata leo, Zakayo hutukumbusha kutubu, na kumrudia Bwana.

Wakati wa huduma yake, dhumuni la Yesu lilikuwa ni watu kumwamini, kumpokea na kumfuata. Pamoja na kukataliwa, lakini wapo wengi waliomwamini, kama Zakayo tuliyemsoma leo ambaye siyo tu kwamba alimpokea, bali alimkaribisha nyumbani kwake, akatoa mali yake kwa maskini, na wale aliowadhulumu akawarudishia mara nne.

Zakayo anakuwa tofauti na ndugu mmoja aliyetaka kumfuata Yesu, alipoambiwa akauze vyote alivyo navyo akaondoka kwa huzuni maana alikuwa na mali nyingi. Huyu alitaka uzima wa milele bila kubadili maisha yake! (Luka 18:18-23). Funzo kubwa hapa ni kugeuza nia zetu na kumfuata Kristo kwa ukamilifu.

Zakayo;

Habari hii hupatikana katika injili ya Luka, na ni maarufu sana miongoni mwa waaminio. Alikuwa mtoza ushuru, hivyo alichukiwa sana. Watoza ushuru walichukiwa kwa sababu walionekana wasaliti, maana walitumikia serikali ya kirumi. Nafasi yao pia iliwawezesha kuwakadiria watu kodi zaidi, hivyo kuwaonea. Walikuwa matajiri. Kwa hiyo jamii ya kiyahudi ilimuona mwenye dhambi. 

Katika somo, mstari wa tatu unaonesha kuwa Zakayo alitamani kumuona Yesu. Sidhani kama mtu anaweza kutamani jambo kwa siku moja. Lazima atakuwa amelisikia, na kutafiti na kujua  zaidi. Hivyo inawezekana Zakayo alikuwa amesikia habari za Yesu muda mrefu, jinsi alivyowapenda watu wote, hata wenye dhambi, sasa alikuwa akimtafuta. Ndipo akakimbia kupanda mti amuone maana alikuwa mfupi. Ipo tafakuri hapa, kuwa Zakayo alisikia neno, akalifanyia kazi. Alisikia habari za Yesu aokoaye, akamtafuta. Hali ikoje kwetu? Ni muda mrefu tumesikia habari za Yesu. Tunamfuata ipasavyo? Hoja kubwa hapa ni kuwa Zakayo alitambua dhambi akatubu. Tunayo toba ya kweli?

Yesu alikuwa akipita Yeriko kuelekea Yerusalemu kwenye adhimisho la Juma kuu. Wengi toka Galilaya walikuwa wakielekea Yerusalemu kwa ajili ya Pasaka. Yeriko ilikuwa njia kuu katika eneo la utawala wa Rumi, na eneo muhimu la kukusanya kodi, huenda ndio maana Zakayo alikuwa tajiri. Wakati ule wakitawaliwa na Warumi, Wayahudi hawakupenda hata kidogo. Walijiona hawako huru. Walikuwa hawana namna, zaidi ya kutii mamlaka ya warumi, ikiwemo kulipa kodi, kiongozi wa wakusanyaji akiwa Zakayo. Wakusanya kodi hawakupendwa, na kwa sababu  hiyo hawakuwa maarufu. Huenda Zakayo alifahamika kwa sababu alikuwa kiongozi wa watozaushuru. 

Chuki dhidi  ya utawala wa waRumi, na chuki dhidi ya watoza ushuru, vilisababisha Yesu aonekane kuingia na kukaa kwa mwenye dhambi. Hapa ndipo Yesu anapoonesha kuwa yeye alikuja kwa ajili ya wenye dhambi. Yesu alilisema hili katika injili zote zinazofanana, akifananisha mgonjwa na mwenye dhambi, kuwa mgonjwa ndiye huhitaji tabibu; Leo tuchukue kwenye Luka;

Luka 5:31

Yesu akajibu akawaambia, Wenye afya hawana haja na tabibu, isipokuwa walio hawawezi.

-Kumbe Yesu alikuja kwa ajili ya wenye dhambi, ndiyo maana hakumpita Zakayo. Ukimtafuta Yesu hakupiti. 

Zakayo alitubu, akampokea Yesu.

Tafakari ya Zakayo inayo mambo mengi ya kuyaangalia. Kwa kuyaangazia machache;

1.Uadilifu kazini na maishani kwa ujumla.

Zakayo alikuwa mtoza ushuru, tena kiongozi wa watoza ushuru. Utaratibu ulikuwa ni watoza ushuru kukadiria kodi kwa walipakodi. Walitumia mwanya huo kukadiria kodi kubwa wakiwaumiza walipa kodi. Ilisababisha pamoja na watoza ushuru kuonekana wasaliti kwa kuwatumikia warumi, wachukiwe pia kwa sababu ya dhuluma katika kukusanya kodi. Ndio maana walikuwa matajiri, kama Zakayo tuliyemsoma. 

Hata leo, siyo wakusanya kodi tu, bali sisi sote tunakumbushwa kutenda haki katika nafasi zetu pasipo kuwaumiza wengine. Unapotoa huduma hapo ulipo, tenda haki. Acha rushwa, chuki, uonevu, upendeleo na mengine kama hayo. Huo ndio utume mwema.

2.Zakayo alikuwa na sifa mbaya.

Kama tulivyoona, Zakayo alikuwa na sifa ya kudhulumu watu. Kwa ujumla, watoza ushuru walikuwa watu waliotolewa mfano mbaya, mfano;

Mathayo 18:17

Na asipowasikiliza wao, liambie kanisa; na asipolisikiliza kanisa pia, na awe kwako kama mtu wa mataifa na mtoza ushuru.

-Mtoza ushuru alionekana wa mataifa. 

Kumbe tunahitaji kujichunguza kama maisha yetu yanamhubiri  Kristo, au ni mfano mbaya. Maisha yako ni ushuhuda mwema au mfano mbaya? Kuwa mfano mbaya hakumzuia Zakayo kutubu. Unangoja nini?

3.Tunaweza kufanywa safi kama Zakayo.

Yesu aliwahi kuwaambia watoza ushuru jinsi ya kuwa safi;

Luka 3:12-13

12 Watoza ushuru nao wakaja kubatizwa, wakamwuliza, Mwalimu, tufanye nini sisi?

13 Akawaambia, Msitoze kitu zaidi kuliko mlivyoamriwa.

Zakayo ni jina, kwa Kiyunani na Kihebrania (Zakkaios) tafsiri yake ni safi, asiye na hatia (pure, innocent). Alikuwa na jina zuri, lakini maisha yake hayakuakisi jina lake. Sisi tumempokea Yesu kwa njia ya ubatizo. Yesu hututangazia msamaha wa dhambi. Pia tunampokea kwa njia ya sacrament ya madhabahu. Je, tunaishi kwa usafi kama tulivyompokea? Kama Zakayo alivyokuwa na jina zuri, nasi tumeitwa na Kristo. Tuko wasafi?

4.Hatuna haja ya kupanda mti kuijua kweli.

Ilimbidi Zakayo kupanda mti ili amwone Yesu. Alikuwa mfupi, na watu walikuwa wengi. Mazingira ya kumwona Yesu yalikuwa magumu zaidi. Alitakiwa kufanya jambo la ziada, kupanda mti. 

Sisi tunahitaji kupanda mti leo kumwona Yesu? Tuna mazingira magumu kiasi hicho?

Katika kuutafuta ufalme wa Mungu, watu walifanya mambo tofauti, mfano;

Watu wa Agano la kale walitoa sadaka ya kuteketezwa. 

Yesu alishaondoa hiyo.

Sisi hatuhitaji kuhangaika. Wala hakuna kisingizio cha aina yoyote. Injili inahubiriwa Kanisani na sehemu nyinginezo kama inavyoandaliwa na Kanisa. Wajibu wetu ni kutubu na kumfuata Kristo. Huna kisingizio. Mpe Yesu maisha yako.

5.Yesu anabisha kuingia kwetu.

Yesu hafurahishwi na njia zetu mbaya. Ndiyo maana Kanisa limeweka utaratibu kwa waamini kuingia Kanisani kwa ibada kila wakati, ili kumsikia Mungu akinena mara nyingi. Anatujia kila wakati. Hata leo anabisha kwetu. Upendo wake ni dhahiri, ndiyo maana alipomwona Zakayo, alimwambia ashuke. 

Inawezekana Zakayo alikuwa na wasiwasi kumkaribisha Yesu nyumbani. Yesu hakungoja kukaribishwa, alimwambia;

Luka 19:5

Na Yesu, alipofika mahali pale, alitazama juu, akamwambia, Zakayo, shuka upesi, kwa kuwa leo imenipasa kushinda nyumbani mwako.

Siyo kushuka tu, alimwambia "shuka upesi". 

Huu ni wito kwetu leo;

Acha uongo upesi

Acha wizi upesi

Acha uzinzi upesi

Acha uonevu upesi 

Acha usengenyaji upesi n.k

Tafakari nini kinakuzuia Yesu kuingia nyumbani kwako; " kiache upesi". Yaani tubu dhambi zako, Yesu anakungoja, maana ahadi yake ni msamaha kwa kila atubuye. 

6.Zakayo alijisalimisha kwa Yesu;

Matendo yasiyompa Mungu utukufu ni ubatili mtupu. Hayafai nyumbani, kazini na Kanisani. Hayafai duniani na mbinguni. Mwisho wake ni kilio  na kusaga meno. 

Kujisalimisha kwa Yesu ndiyo njia sahihi kuelekea uzima wa milele. Nini uamuzi wako katika hili?

Mruhusu Yesu aingie kwako, atakase nyumba yako.

Bwana akubariki 

Heri Buberwa Nteboya 

0784 968650

bernardina.nyamichwo@gmail.com