
Alhamisi asubuhi tarehe 22.10.2026;
Ezekieli 34:9-10
9 kwa sababu hiyo, enyi wachungaji, lisikieni neno la Bwana;
10 Bwana MUNGU asema hivi; Tazama, mimi ni juu ya wachungaji; nami nitawataka kondoo zangu mikononi mwao, nami nitawaachisha hiyo kazi ya kuwalisha kondoo; nao wachungaji hawatajilisha wenyewe tena; nami nitawaokoa kondoo zangu vinywani mwao, wasiwe tena chakula chao.
Madhara ya kudharau wito;
Nabii Ezekieli anatumia mfano wa Mchungaji kuelezea jinsi viongozi wa Israeli walivyoshindwa kuwaongoza na kuwatunza watu wa Mungu. Viongozi (wachungaji) waliwakandamiza watu (kondoo) kwenye taifa walilopewa na Mungu. Viongozi hawa waliongoza bila kujali watu, walijinufaisha wao kwa maslahi binafsi. Angalia hapa;
Ezekieli 34:2-3
2 Mwanadamu, toa unabii juu ya wachungaji wa Israeli, toa unabii, uwaambie, naam, hao wachungaji, Bwana MUNGU asema hivi; Ole wao wachungaji wa Israeli, wanaojilisha wenyewe; je! Haiwapasi wachungaji kuwalisha kondoo?
3 Mnawala walionona, mnajivika manyoya, mnawachinja walionona; lakini hamwalishi kondoo.
Mungu anawaonya waliowaacha kondoo wakatawanyika, hadi wengine kuwa chakula cha mbwa mwitu! Ujumbe huu kwa Kanisa la leo unatukumbusha kuwa sote tuna wajibu wa kuitenda kazi ya Bwana, tukiwaleta watu kwa Yesu Kristo aliye Mchungaji mwema. Tunatekeleza?
Siku njema
Heri Buberwa
