1 Wafalme 17:10-16 - 25-07-2026

Date
Reading
1 Wafalme 17:10-16

Jumamosi asubuhi tarehe 25.07.2026;

1 Wafalme 17:10-16

10 Basi, akaondoka, akaenda Sarepta; hata alipofika langoni pa mji, kumbe! Mwanamke mjane alikuwako akiokota kuni; akamwita, akamwambia, Niletee, nakuomba, maji kidogo chomboni nipate kunywa.

11 Alipokuwa akienda kuleta, akamwita akasema, Niletee, nakuomba, kipande cha mkate mkononi mwako.

12 Naye akasema, Kama Bwana, Mungu wako, aishivyo, sina mkate, ila konzi ya unga katika pipa, na mafuta kidogo katika chupa; nami ninaokota kuni mbili ili niingie nijipikie nafsi yangu na mwanangu, tuule tukafe.

13 Eliya akamwambia, Usiogope; enenda ukafanye kama ulivyosema; lakini unifanyie kwanza mkate mdogo ukaniletee; kisha ujifanyie nafsi yako na mwanao.

14 Kwa kuwa Bwana, Mungu wa Israeli, asema hivi, Lile pipa la unga halitapunguka, wala ile chupa ya mafuta haitaisha, hata siku ile Bwana atakapoleta mvua juu ya nchi.

15 Basi akaenda, akafanya kama alivyosema Eliya; na yeye mwenyewe, na Eliya, na nyumba yake, wakala siku nyingi.

16 Lile pipa la unga halikupunguka, wala ile chupa ya mafuta haikuisha, sawasawa na neno la Bwana alilolinena kwa kinywa cha Eliya.

Neema ya Mungu yatosha;

Ni habari ya mwanamke mjane mmoja huko Sarepta ambaye alikutwa na Eliya akiokota kuni, Eliya akamtaka kumpa mkate. Yule mama akasema hakuwa na mkate, bali unga kidogo na mafuta kidogo. Eliya akamwambia asiogope, akamtengenezee mkate kwanza. Yule mama akatengeneza mkate akampa Eliya. Eliya akampa unabii wa kutopungukiwa chakula nyumbani mwake hadi Bwana atakapoleta mvua juu ya nchi. 

Yule mwanamke alikuwa na wasiwasi, kwamba baada ya pale angekufa yeye na mwanae maana wasingekuwa na chakula tena. Lakini kama Eliya alivyosema, hawakukosa tena chakula. Neema ya Mungu ilikuwa juu yao hata kutokufa kwa njaa. Kwa neema ya Mungu nasi tunayaweza yote katika yeye aliyetuita. Tusiondoke kwake, yaani tusiiache imani maana ndiyo njia sahihi kuelekea uzima wa milele. Amina

Jumamosi njema

Heri Buberwa